Yesu na Mohamed pembeni kwanza

Yesu na Mohamed pembeni kwanza

britanicca

Platinum Member
Joined
May 20, 2015
Posts
18,421
Reaction score
50,351
Habari za Jumapili ni Encyclopedia Tena nina ka debate kidogo

UTU KABLA YA DINI: Maadili Hayakuanza na Vitabu


Kuna swali ambalo watu wengi hawaulizi kwa sauti, lakini mioyoni mwao wanajiuliza kila siku:

Kama dini ndiyo iliyotuletea maadili, basi watu wa kabla ya dini waliishije?

Ukiweka akili yako mezani, bila kushikiliwa na hofu wala mila uliyorithi, utagundua ukweli mmoja ambao unatikisa misingi mingi: Wema ulikuwepo kabla ya dini. Dini haikuja kuumba wema, ilikuja kuukuta wema ukishakuwepo.

Kabla ya Bwana Yesu hajaja, na kabla ya miaka 600 kupita kisha Mohamed hajajitokeza, dunia ilishakuwa na mabilioni ya watu. Walioana, walizaa, walijenga vijiji, walilima, walivua samaki, walitunza wagonjwa na walizika wafu wao kwa heshima. Je, waliishi kama wanyama? Hapana. Waliishi kwa sheria ambazo hazikuandikwa kwenye vitabu, bali ziliandikwa kwenye mioyo yao.

Hizi hapa ni sheria 11 ambazo ziliwatawala watu kabla ya dini:

1. Hawakupenda Wizi

Katika jamii ya zamani, hakuna polisi, hakuna kamera, hakuna mahakama ya kisasa. Lakini mwizi alikuwa adui wa wote.

Kwa nini? Kwa sababu kila mtu alijua hesabu rahisi: Leo umeniibia mimi, kesho utamuibia mwingine, kesho kutwa jamii nzima itakuwa haiaminiwi na tutakufa njaa.

Kule Katika kijiji cha Wasukuma zamani, mtu akivuna mahindi yake akayaweka nje kukauka, hakuna aliyegusa hata punje moja. Sio kwa sababu aliogopa adhabu ya Mungu, bali aliogopa aibu. Mwizi akishikwa, jina lake lilihariwa vizazi vitatu mbele. Aibu ilikuwa adhabu kubwa kuliko jela.

Wizi ulichukiwa sio kwa sababu ya amri, bali kwa sababu unavunja uaminifu ambao jamii inasimama juu yake.

2. Hawakupenda Kuchepuka na Wake za Watu

Uzinzi ulikuwa ni kitendo cha kuvunja amani.

Mwanaume aliyemchukua mke wa mwenzake alijua wazi kuwa anaanzisha vita. Familia mbili zitagombana, watoto watabaki yatima wa kiroho, na kijiji kizima kitapoteza amani.

Natoa mfano Kwa Wamasai, mke wa mtu ni heshima ya ukoo mzima. Kumuingilia ni sawa na kuingia kwenye nyumba ya mtu na kumchukua mkuki wake. Ni vita. Hii haikufundishwa na dini, ilifundishwa na maisha yenyewe.

3. Hawakupenda Kuua Wenzao

Kabla ya amri "Usiue" haijaandikwa popote, watu walishajua kuua ni uharibifu.

Jamii ndogo ya watu 50 ikipoteza mtu mmoja kwa mauaji, imepoteza mwindaji, mlinzi, baba, na nguvu kazi. Kumuua mwenzako ilikuwa sawa na kujikata mkono wako mwenyewe.

Let say Kama kijijini kuna simba anawavamia mifugo, unahitaji watu 10 wenye mikuki kwenda kumshinda. Ukimuua mmoja kati yao jana kwa hasira, leo simba atawala. Hivyo, kuua kulikatazwa na akili, sio na vitabu.

4. Hawakuwadharau Wazazi

Wazee walikuwa ndiyo shule, hospitali, na kalenda ya kijiji.

Wao ndio waliojua ni mti gani unatibu malaria, ni wapi maji yapo wakati wa kiangazi, na ni lini mvua itanyesha. Kumdharau mzazi kulikuwa ni kama kuchoma maktaba ya kijiji kizima.

Mtoto aliyemtukana baba yake hakuadhibiwa na Mungu kwanza, aliadhibiwa na kijiji. Kijiji kilimwambia, "Huyu kesho atatutukana sisi pia." Heshima kwa wazazi ilikuwa ni akili ya kuishi.

5. Waligawiana Kidogo Walicho Nacho Wakati wa Shida na Raha

Huu ndio msingi wa Ujamaa kabla ya Ujamaa kuitwa jina.

Wawindaji wakipata swala mmoja, hawakula peke yao. Waligawa nyama kwa wote, hata kwa wale wasiokwenda kuwinda siku hiyo.

Kwa nini? Kwa sababu walijua sheria ya porini: Leo ni zamu yangu kupata, kesho ni zamu yako kunisaidia.

Mfano
: Mvuvi wa Zanzibar akivua samaki wengi, anawapa majirani kwanza kabla hajauza. Anajua kesho bahari inaweza kuwa mbaya kwake, na yeye ndiye atahitaji kupewa. Kugawana sio dini, ni bima ya maisha.

6. Hawakupenda Uongo

Uongo ulionekana kama sumu ya jamii.

Kama mtu akisema "Wanyama wamekuja shambani" wakati ni uongo, kesho akisema kweli hakuna atakayemwamini. Na siku ambayo simba wa kweli atakuja, wote watakufa kwa sababu wameshazoea uongo wake.

Mfano Kijijini, mtu mwongo alipewa jina la "mwongo" na hakuna aliyempa binti yake kuoa. Sio kwa sababu dini imesema, bali kwa sababu kijiji hakiwezi kujengwa juu ya uongo.

7. Hawakupenda Anayemuonea Wivu Mwingine

Wivu ulichukuliwa kama ugonjwa wa moyo unaoweza kuua kijiji.

Mtu mwenye wivu anaweza kuchoma nyumba ya jirani yake, kumroga mtoto wake, au kumsingizia. Jamii ilijua, mtu mwenye wivu ni hatari zaidi ya simba.

Hivyo walimweka pembeni. Walimfundisha, wakimshindwa, walimtenga ili kulinda amani ya wote.

8. Walipenda Kuombana Msamaha Walipokoseana

Kabla ya neno "toba" halijafika, kulikuwa na desturi ya kukaa chini chini ya mti mkubwa.

Mkosaji alikiri: "Nimekosea."
Mkoswaji alijibu: "Nimekusamehe."

Bila desturi hii, kisasi kisingeisha. Kabila moja lingeua kabila lingine, na lingine lingelipiza kisasi, mpaka wote waangamie. Msamaha ulikuwa sio kitendo cha kidini, ulikuwa ni kitendo cha kuokoa kizazi.

9. Waliishi Kwa Upendo Na Ambaye Alionekana Kutokuwa Na Upendo Alitengwa

Mtu asiyejali, asiyewasaidia wajane, asiyewabeba wagonjwa, asiyecheka na watoto, alionekana kama mtu aliyekufa akiwa hai.

Jamii ilimpa nafasi ya kubadilika, ikishindwa, ilimtenga. Sio kwa chuki, bali kwa kulinda watoto wasiige tabia ya ukatili.

10. Hakuna Aliyemlala Ndugu au Jamaa Yake

Hii ilikuwa sheria ya asili duniani kote. Kuanzia Amerika ya Kusini hadi Asia, kila kabila lilikataza ndoa za damu.

Waliona kwa macho: watoto wanaozaliwa kwenye ndoa za ndugu wanazaliwa dhaifu, wagonjwa, na familia inavunjika. Sayansi ya leo, yaani genetics, inathibitisha kile walichokijua kwa uzoefu miaka elfu iliyopita.

11. Mtu Asingemuingilia Mwingine Kinyume na Maumbile Akachekewa, Ilikuwa Hawapendi

Jamii za kale ziliamini familia ni msingi wa kila kitu. Kitu chochote kilichoonekana kuvunja muundo wa familia na heshima ya mwili wa mwanadamu, hakikuchukuliwa kama jambo la kuchekelewa. Kilichukuliwa kwa uzito, kwa sababu walijua kama familia ikivunjika, taifa linavunjika.


SASA SWALI LANGU NI HILI:

Kama haya yote yalikuwepo, kwa nini tunashangaa leo kwamba ujio wa dini umeonekana kukoleza na kuyatangaza maovu zaidi?

Leo tunasikia wizi ukiwa umevalishwa joho la dini. Uongo ukiwa umefunikwa na mahubiri mazuri. Mauaji yakiwa yameitwa "kazi ya Mungu". Wivu na chuki zikiwa zimeitwa "sisi ndio wenye ukweli, wengine ni wapotevu".

Inaonekana kama badala ya dini kutuondolea maovu, wakati mwingine imeyapa maovu hayo nguvu mpya, na jina jipya la heshima. Mtu anaweza kuiba, halafu akisema "Mungu amenibariki" watu wanamshangilia. Mtu anaweza kudanganya, halafu akisema "nimemwona Mungu ndotoni" watu wanamsikiliza.

Hii ndiyo inayonishangaza.

NIMEKAA NA WASIO NA IMANI

Nimejaribu kukaa na watu wasioamini uwepo wa Mungu kabisa, wale wanaoitwa Atheists.

Nilitegemea nitakuta watu wabaya, wenye chuki, wanaopenda dhambi. Lakini nimekuta kinyume chake.

Nao wanachukia wizi. Nao wanachukia uongo. Nao wanawapenda wazazi wao. Nao wanasaidia maskini. Nao wanaomba msamaha wakikosea.

Hii imenifundisha kitu kikubwa:

UTU NI MKUBWA KULIKO DINI.

Utu uko ndani ya mwanadamu. Dini inaweza kutukumbusha, inaweza kututia moyo, lakini haikutuumba kuwa wema. Tulikuwa wema kwa sababu tunahitajiana ili tuishi.

Kama leo tungeondoa vitabu vyote, watu wasingependa kuua ghafla. Kama tungeondoa misikiti na makanisa yote, mama asingeacha kumpa mtoto wake maziwa. Kwa sababu moyo wa mwanadamu unajua jema na baya kabla kitabu hakijamwambia.

HITIMISHO

Siamini kwamba dini haina maana. Dini ina nafasi yake ya kututia tumaini na kutuunganisha.

Lakini nataka tusikubali kudanganywa kwamba bila dini, mwanadamu ni mnyama. Historia inasema kinyume. Mwanadamu alikuwa mwanadamu kabla ya dini, na atabaki mwanadamu baada ya dini.

Wema sio wa Wakristo tu, sio wa Waislamu tu, sio wa wenye imani tu. Wema ni wa wanadamu wote.

Na kama kweli tunataka dunia nzuri, tusianze kwa kuuliza "Wewe una dini gani?" Tuanze kwa kuuliza "Wewe una utu kiasi gani?"

Kwa sababu mwisho wa siku, Mungu kama yupo, hatatuuliza tulikuwa na dini gani. Atatuuliza tulimtendea vipi mwenzetu.

Nimejiuliza sana

Anaua leo au anatoa amri ya kuua lakin Kesho Mgeni rasmi msikitini na anafuturisha

Anaua leo Ila Kesho ana kanisa lake naye anahubiri na analia kwamba anahisi wokovu

Anaua leo Kesho kutwa kibaraghashia ana hadaa waumini
Britanicca
 
Ukitimia akili bila kushikiwa utayataka yale mazuri yanayofundishwa kutoka kila upande, hata kabla ya Ujio wa


Britanicca
Screenshot_20260816-150515~2.png
 
Nikubaliane nawe katika historia ya binadamu ulio ieleza. Kifupi dini zimeleta uvunjifu wa amani na mfarakano zaidi. Zimeleta utengano badala ya mshikamano. Ndugu mkristu na mwislamu ni watu mbali. Na bahati mbaya bado wengi hawajaelewa chimbuko la dini. Itachukua muda, lakini itafika muda, milango ya makanisa na misikiti itafungwa.
 
Kabla Yesu hajavaa mwili wa mwanadamu alikuwepo , maana ndiye Mungu.

Sàsa unawezaje kuweka kando?
 
Yawezekana mwandishi alitaka kusema kabla ya Torati, Zaburi, Injili na Korani binadamu waliishi kwa upendo, kushirikiana, kusaidiana na kwa utulivu na amani. Haki ilizingatiwa na mabaraza ya wazee yalikuwa yakitumika kuhakikisha haki inapatikana na uonevu hautamalaki. Kinachotuvuruga leo ni ushabiki wa kisiasa (kugombania madaraka) ambao umeingizwa kwenye dini na ndiyo sababu tunashuhudia vita na umwagaji damu mwingi kwenye baadhi ya mataifa yenye waislamu au wakristu pekee.
 
Back
Top Bottom