Sikuikifika,
Asante kwa maoni yako. Naelewa wajibu wa mbunge na nililieleza hili bayana mwanzoni mwa mwaka huu wakati natangaza dhamira ya kugombea:
Nanukuu: Naamini kwamba mbunge (ambaye pia kwa nafasi yake ni diwani katika halmashauri) ana wajibu katika maeneo makuu manne (kwa kadiri ya umuhimu).
Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.
Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.
Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria unaosubiriwa kutungiwa kanuni. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa mtoa bidhaa na huduma (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla." Unaweza kujikumbusha kauli yangu kwa ukamilifu wake hapa:
https://www.jamiiforums.com/jukwaa-...-rasmi-dhamira-ya-kugombea-ubunge-2010-a.html
Naelewa kwamba maoni yako yametokana na Hotuba yangu ya tarehe 12 mwezi 12 Kwenye kongamano la maendeleo jimbo la Ubungo ambapo nilitangaza kwamba nimeshaanza kutekeleza ahadi yangu ya kwenye kampeni ya kutenga 20% ya mshahara wangu kwa mwezi kuingiza kwenye mfuko wa Elimu Ubungo ili kuhamasisha wadau wengine nao kuuchangia. Kwenye kongamano hilo wakati najibu mada zilizotolewa na vijana wasomi hususani wazo la kuwa na kituo cha elimu kwa umma nilisema kwamba mpaka kwa pamoja mimi na wao tutakapofanikisha kuanzisha kituo husika binafsi nitaoongoza harakati hizo kwa kutoa 20 % ya posho kwa kipindi chote cha uhamasishaji mpaka kazi itakapokamilika. Nilifanya hivyo nikijua bayana majukumu ya mbunge- lakini nilifanya hivyo kama sehemu ya kuonyesha kwa vitendo kwamba ukijumuisha mishahara na posho kwa mwezi wabunge wanalipwa zaidi ukilinganisha na watumishi wengine wa umma kama walimu, maaskari nk; hivyo nimeamua kurudisha sehemu ya kodi hizo za wananchi kwa wananchi wenyewe kupitia jitihada za pamoja za kuleta maendeleo. Nakukaribisha na wewe utuunge mkono katika harakati zetu ubungo; tutaibana serikali, lakini na sisi wenyewe tunajibana.
JJ