NMB yapata Mkurugenzi mpya
Send to a friend Wednesday, 12 January 2011 20:14
Mark Wiessing
Furaha Maugo
BODI ya wakurugenzi ya Benki ya Makabwela (NMB), imemteua Mark Wiessing kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo.
Wiessing ameshika nafasi hiyo kutoka kwa Ben Christiaanse ambaye amememaliza muda wake wa miaka minne.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Misheck Ngatunga, alisema Wiessing ni mchapakazi na ana uzoefu.
Anakuja na uzoefu mkubwa wa masuala ya kibenki, uzoefu alioupata sehemu kubwa ya Afrika na sehemu nyingine duniani hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na ongezeko kubwa la ushindani katika soko, alisema Ngatunga.
Wiessing(52)kabla ya kushika wadhifa huo amewahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa Benki Taifa ya Biashara Zambia(ZANACO),Standard Charted nchini Afrika Kusini, amewahi pia kuwa ,Mkurugenzi wa Kanda ya nchi za Afrika Magharibi katika shughuli za kibenki.
Amewahi kuwa Mratibu wa City Bank nchini Ivory Coast, amefanyakazi nchi za Ulaya Mashariki,Kusini Mashariki mwa Asia na kampuni ya IGP.
Ana Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara aliyopata chuo kikuu cha USA.
Benki ya NMB ilianzishwa mwaka 1997 lakini mwaka 2005 ilibinafsishwa baada ya serikali kuuza asilimia 49 ya hisa zake kwa Rabobank.
Mwaka 2008 serikali ilipunguza tena hisa zake hadi kufikia asilimia 30, kwa kuuza hisa za asilimia 16 kwa wananchi na asilimia 5 kwa wafanyakazi wake, ambapo mwaka huohuo iliorodheswa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).