Date: 9/22/2008
Takukuru yachunguza sita BoT
*SASA YAFANYA UCHUNGUZI WA RUSHWA
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
BAADA ya uongozi wa Benki Kuu (BoT) kuchukua hatua za kinidhamu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inawachunguza vigogo sita wa benki hiyo, kutokana na tuhuma za rushwa katika fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Uchunguzi huo wa Takukuru umekuja wakati tayari ikiwa imefanya uchunguzi wa watoto 16 wa vigogo, ndani ya BoT na uchunguzi wa gharama za ujenzi wa majengo pacha (Twin Tower) ya ghorofa 18.
Taarifa kutoka ndani ya BoT zinasema baada ya jopo la kamati ya nidhamu ya benki hiyo kumaliza kazi kwa kuadhibu vigogo sita, wakiwemo wakurugenzi, Takukuru imejiingiza kuchunguza makosa ya jinai ya rushwa.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, alipoulizwa suala hilo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, alisema hiyo ni kazi ya Takukuru kwani mwisho wa kazi ya benki ni kutoa adhabu za kinidhamu.
Lakini Profesa Ndulu akabainisha kuwa BoT imetoa taarifa ambazo Takukuru imekuwa ikihitaji kuhusu maafisa wa EPA.
"Sisi (BoT) hutuhusiki na jinai, kazi yetu ni kuchukua hatua za kinidhamu, hayo mambo ya jinai si yetu, lakini Takukuru tumekuwa tukiwapa taarifa wanazohitaji," alisema kwa kifupi Profesa Ndulu na kuongeza:
"Hata katika uchunguzi wa ajira za baadhi ya watumishi wanaodaiwa kughushi, sisi tulichukua hatua zetu na wao za kwao za jinai, sasa ni vema ukawatafuta wenyewe."
Hata hivyo, kifungu cha 37 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Takukuru ya mwaka 2007, inazuia taasisi hiyo kuzungumzia uchunguzi unaoendelea.
Habari hizo kutoka BoT zilifafanua zaidi kwamba, Takukuru inawachunguza maafisa hao kuona kama wamenufaika na fedha za EPA.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, vigogo hao iwapo watabainika kunufaika na fedha hizo huenda wakakabiliwa na makosa ya jinai ya rushwa.
"Lengo kubwa ni kuona kama wamenufaika kwa namna moja au nyingine, sasa kama wamenufaika wanaweza kukabiliwa na mashitaka ya jinai," alisema mtu mmoja kutoka BoT.
Chanzo kingine kutoka BoT kilieleza kwamba maafisa hao ambao wametajwa katika Ripoti ya Ukaguzi ya Ersnt & Young, wanachunguzwa kwa jinai huku rufaa zao za adhabu za kinidhamu zikiwa katika hatua ya mwisho.
Rufaa nne kutoka kwa vigogo hao sita, akiwemo mkurugenzi mmoja ambaye mkataba wake wa kustaafu ulikwisha mwezi Machi, zinasikilizwa na mwenyekiti wa rufaa, ambaye kwa sheria ya BoT ni Gavana.
Chanzo hicho kilifafanua zaidi kwamba, vigogo hao sita kwa sasa wako kwenye wakati mgumu kutokana na kwamba, walitajwa katika ripoti ya ukaguzi wa kitaalamu.
"Kinachowapa hofu ni kwamba, kwanza tayari wametajwa katika ripoti ya ukaguzi wa Ernst & Young, ndiyo maana hata BoT ilipowachukulia hatua za kinidhamu, ilipitia ripoti hiyo na kisha yenyewe kufanya uchunguzi wa kina na kujiridhisha kwamba kwa namna moja au nyingine walihusika," kilisema chanzo hicho na kuongeza:
"BoT haikukurupuka hata kidogo... yule gavana (Profesa Ndulu), ni mtu makini sana... wafanyakazi wengi wanampenda, hapendi majungu, ndiyo maana nakwambia hawa jamaa hadi kuadhibiwa ujue kumefanyika uchunguzi wa kweli."
Chanzo hicho kiliongeza kwamba, mkurugenzi wa sita ambaye ameingizwa katika orodha hiyo alikuwa amestaafu Machi lakini naye ameingizwa katika orodha na anachunguzwa, kwani wakati ufisadi ukitokea mwaka 2005/06, alikuwepo.
"Sasa hapa ndipo utajua hawa watu wana wakati mgumu, huyu mkurugenzi alimaliza mkataba wake mwezi Machi, lakini ameingizwa katika orodha kwani wakati wizi ukitokea alikuwepo katika madaraka," kilifafanua chanzo kingine.
Tuhuma za ufisadi katika akaunti ya EPA ziliibuliwa katika ukaguzi wa hesabu za mwaka 2005/06 uliofanywa na Ersnt&Young, baada ya ule wa Kampuni ya Deloitte&Touche ya Afrika Kusini kusitishwa.
Baada ya Deloitte&Touche kubaini ufisadi uliofanywa na Kampuni ya Kagoda, ghafla ilisitishiwa mkataba, hali iliyozidisha maswali ambayo yaliibua mjadala mzito bungeni hadi serikali kuagiza uchunguzi ufanywe na Ersnt& Young, ambayo iliibua kashfa hiyo ya wizi wa zaidi ya Sh133 bilioni.
Baada ya kubaini ufisadi huo, Januari mwaka huu Rais Jakaya Kikwete, aliagiza hatua zichukuliwe kwa wahusika ndani ya BoT kwa mujibu wa taratibu za benki.
Kufuatia agizo hilo, kwa mara ya kwanza Gavana Profesa Ndulu, mwezi Januari alifanya mabadiliko makubwa ya wakurugenzi ambayo yalifuatiwa na kung'olewa vigogo hao sita wa sasa.
Katika mabadiliko ya Januari, Profesa Ndulu alibadili wakurugenzi kutoka idara mbalimbali isipokuwa Uchumi, Fedha na Masoko.
Katika mabadiliko hayo, gavana huyo ambaye amekuwa akiangaliwa kama mwenye kuweza kuleta mabadiliko ndani ya BoT kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi Benki ya Dunia (WB), alisafisha wakurugenzi wa Idara za Makao Makuu na matawi yote ya benki hiyo, isipokuwa Mwanza.
Matawi ya BoT nchini ukiacha Mwanza ni pamoja na Zanzibar, Mbeya na Arusha ambayo yamekuwa yakiongozwa na wakurugenzi.
Idara zilizokumbwa na mabadiliko hayo ni Utawala na Utumishi, Fedha, Benki, Idara inayoshughulikia Deni la Taifa na inayoshughulikia Zabuni.